Askofu wa jimbo Katoliki la Eldoret Rt. Rev. Dominic Kimengicha ametoa wito kwa viongozi nchini kusitisha malumbano ya kisiasa na badala yake kuelekeza juhudi zao katika kuangazia janga la Corona.
Kwenye homilia yake wakati wa Misa ya Jumapili ya kuadhimisha sherehe ya Kupaa Kwa Bwana katika kanisa la Holy Family Basilica jijini Nairobi, askofu Kimengich amesema huu sio wakati wa viongozi kuanza kuzozana bali kuonyesha umoja wao katika kuwafaa wakenya wanaopitia wakati mgumu kiuchumi.
Askofu Kimengich amewataka wanasiasa kuto tonesha vidonda vya uhasama wa kisiasa miongoni mwa wakenya kwa kuanza siasa za migawanyiko sawia na zile zinazoshuhudiwa ndani ya chama cha Jubilee kuhusu nyadhifa za uwakilishi bungeni.
Wakati uo huo amewahimiza wakenya kutokata tamaa wakati huu wa janga la Corona bali kuendelea kumwomba Mungu ili kurejelea maisha yao ya kawaida huku pia akiwatakia waislamu wote Eid-Mubarak.
