Italia imeongeza hatua za dharura za kupambana na maambukizi ya virusi vya corona, ikiwemo kuzuia safari na kupiga marufuku mikusanyiko ya Umma nchi nzima.
Siku ya Jumatatu, Waziri Mkuu Giuseppe Conte aliamuru watu wabaki majumbani na sharti waombe ruhusa na kupata kibali kwa ajili ya safari zenye umuhimu pekee.
Amesema hatua hizo ziliwekwa kwa ajili ya kuwalinda wale walio hatarini kupata maambukizi . Vifo vilivyotokana na virusi vya corona sasa vimefikia 463 kutoka 366 siku ya Jumatatu. Athari mbaya zaidi baada ya China.
Idadi ya maambukizi imethibitishwa kufikia 24% kutoka siku ya Jumapili, maafisa walieleza.Visa vya maambukizi vimethibitishwa kuwepo kwenye miji yote 20 nchini Italia.
Waziri Mkuu Conte ameeleza hatua hiyo inajulikana kwa jina ”Ninabaki nyumbani”- watu wakipigwa marufuku kukusanyika. Matukio ya michezo ikiwemo mechi za kandanda zimezuiwa nchi nzima. Shule zimefungwa na vyuo vitabaki vimefungwa mpaka tarehe 3 mwezi Aprili.
Serikali imesema wale wenye sababu za kikazi na kifamilia ambazo haziwezi kuahirishwa wataruhusiwa kusafiri.Abiria wanaotaka kuondoka wanatakiwa kuwa na sababu za msingi, kama watakavyofanya wanaoingia na ndege nchini humo.
Kwenye vituo vya treni kuna udhibiti pia, abiria hupimwa kiwango cha joto cha mwili. Meli pia zimezuiwa kutia nanga katika bandari kadhaa nchini humo.