Shirika la Afya Ulimwenguni – WHO limesema leo kuwa sasa kuna visa zaidi vipya vya virusi vya corona vinavyoripotiwa kila siku nje ya China kuliko ndani ya nchi hiyo iliyoathirika pakubwa na janga hilo.
Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amewaambia wanadiplomasia mjini Geneva, kuwa kwa mara ya kwanza, idadi ya visa vipya vya maambukizi ya virusi hivyo nje ya China imezidi idadi ya visa vipya nchini China. WHO imesema kuwa kufikia jana, kulikuwa na visa vipya 411 nchini China na vilivyoripotiwa nje ya nchi hiyo ni 427.
Serikali kote ulimwenguni zinapambana kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo vya corona baada ya kupanda kwa maambukizi nchini Italia, Iran na Korea Kusini. Ghebreyesus amesema kuongezeka kwa visa hivyo kunatia wasiwasi mkubwa na kwamba timu ya WHO itakwenda Iran mwishoni mwa wiki hii kutathmini hali. Mpaka leo asubuhi, WHO inasema kulikuwa na visa 78,190 vya virusi hivyo nchini China, vikiwemo vifo vya watu 2,718.