Jumapili ya kupaa kwa bwana

Katika dominika hii ya leo, Kanisa linaadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana. Sherehe hii ni adhimisho la mojawapo ya mafumbo makuu ya imani yetu kuwa siku 40 baada ya kufufuka, Kristo alipaa mbinguni na huko amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi.

Kristo Yesu baada ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, kwa muda wa siku arobaini aliwatokea wafuasi wake na kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo. Alitumia fursa hii kwa ajili ya kuwaandaa kwa ujio wa Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana. Kanisa ni utimilifu wa Fumbo la Pasaka!

Kristo Yesu Mfufuka kabla ya kupaa kwenda zake mbinguni aliwaambia wafuasi wake kwamba, amepewa mamlaka yote mbinguni na duniani ambayo kimsingi ni nguvu ya Mungu na akawaahidia kuwapatia nguvu ya Roho Mtakatifu yenye utendaji na uweza mkuu unaounganisha mbingu na dunia, hili ndilo haswa Fumbo linaloadhimishwa kwa Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni. 

Papa Mtakatifu Francisko anasema, hii ni Sherehe inayoonesha kutukuka kwa mwili wa binadamu mbele ya Mwenyezi Mungu, kiini cha imani na matumaini kuwa, daima Mwenyezi Mungu ataendelea kuambatana na binadamu na kwamba, mbinguni, kila mtu anaandaliwa makazi ya milele. Kumbe, waamini wanapaswa kuishi hapa duniani wakiwa wanayaambata zaidi yale ya mbinguni, kama alivyofanya KristoYesu kwa kuunganisha mbingu na dunia!

Lakini, waamini wanakumbushwa kwamba, licha ya Kristo Yesu kupaa mbinguni, lakini bado anaendelea kuwa pamoja na waja wake hadi utimilifu wa dahari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *