Serikali ya kaunti ya Uasin Gishu ikishirikiana na mamlaka ya Barbara za mijini KURA wamekagua ukarabati wa barabara ndani ya mji wa Eldoret kwa uboreshaji wa miundomsingi na pia kujitayarisha kwa kongamano la Ugatuzi la 2023 litakalofanyika kuanzia tarehe 15-19 Agosti mwaka huu mjini Eldoret.
Kulingana na taarifa yake mkurugenzi wa mali na usimamizi wa barabara wa KURA ,Mhandisi Abdulrashid Sheikh Mohammed anasema kwamba wasimamizi wa KURA na kaunti wameagana kuweka lami ya jumla ya kilomita 3 ndani ya mji wa Eldoret na hadi wa sasa kilimoti 1.5 tayari imekamilika.
Wakati wa ukaguzi wa barabara hizo ambazo ziko katika wadi ya Racecourse ,Kaunti ndogo ya Kesses ,waziri wa uchukuzi,barabara na maendeleo kaunti hii Mhandisi Joseph Lagat amesema kukamilika kwa barabara hizo kutapunguza msongamano wa magari mjini hasa kwenye barabara zenye shughuli nyingi kama ya Kapsabet-Kisumu.
Waziri pia alisema kwamba mwaka huu kaunti inalenga kukamilisha uwekaji alama wa kilomita 600 za barabara ambapo mwaka jana mpango wa uwekaji alama barabarani ulifanikisha kilomita 800 za barabara za murram na kilomita 400 za changarawe na barabara fupi.
Wakati huo,wenyeji maeneo hayo wakishabikia hatua ya ukarabati na ujenzi wa barabara hizo wakieleza kwamba wataimarika kibiashara na hata usalama.