KCCB yataka vijana kujitenga na uhuni

Baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini KCCB limetoa wito kwa vijana kutokubali kutumiwa na wanasiasa kuzua vurugu nchini.

Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni askofu mkuu wa Jimbo kuu katoliki la Kisumu Maurice Muhatia Makumba, ametoa wito kwa vijana kuwa mabalozi wema wa amani na kujitenga na visa vya uhuni nchini, akisema kuwa swala la uhuni nchini linapaka tope jina la vijana akiwataka kujitenga na jina hilo la uhuni.

Amewataka vijana hao kukataa mwito wa wanasiasa ambao siku zote wana lengo la kuzua vurugu na uharibifu nchini akiwataka kuwa macho na kamwe kutokubali kutumiwa kuvuruga mshikamano wa kitaifa.

Hii inakuja wakati ambapo taifa la Kenya litakuwa mwenyeji wa kongamano la ishirini na Moja la AMECEA, linalojimuisha mataifa tisa wanachama lengo  likiwa ni kuangazia maadili miongoni mwa vijana na namna ya kutembea pamoja na vijana kama kanisa la kisinodi.

Naye askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Nairobi Philip Anyolo amesema kuwa visa hivyo vya wahuni nchini vinastahili kukomeshwa, kwa kuwa vinasambaratisha mshikamano wa kitaifa akitoa wito kwa wanasiasa kunadi sera zao kwa njia ya amani pasi na kutumia wahuni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *