Papa Leo aonya kitisho cha AI kupitia waraka muhimu

Baba mtakatifu Leo wa kumi na nne ametoa waraka wake wa kwanza unaojulikana kama “Magnifica Humanitas”, akitoa onyo kali kuhusu hatari zinazotokana na maendeleo ya kasi ya teknolojia ya akili mnemba (AI).

Waraka huo ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa, hasa baada ya Papa Leo ambaye ni papa wa kwanza kutoka Marekani, kusema siku chache baada ya kuchaguliwa kuwa anaona AI kama changamoto kubwa zaidi inayoukabili ubinadamu kwa sasa.

Katika waraka huo, Papa Leo XIV amekosoa kile alichokiita “utamaduni wa nguvu” unaochochea mashindano ya kimataifa katika maendeleo ya AI. Alionyesha wasiwasi wake hasa kuhusu matumizi ya teknolojia hiyo katika nyanja za kijeshi, akibainisha kuwa inachangia kuibuka kwa njia mpya na hatari za vita vinavyoendeshwa kwa mbali.

Papa Leo alisisitiza kuwa haifai kabisa kuzikabidhi mashine maamuzi yasiyoweza kubadilishwa, hususan yale yanayohusu maisha na kifo. “Si halali kuziachia mifumo ya akili bandia kufanya maamuzi ya kuua, ambayo hayawezi kurekebishwa,” alisema katika waraka huo.

Kauli hiyo inaonekana kuongeza mvutano mpya kati ya Papa Leo na utawala wa Marekani chini ya Rais Donald Trump, ambao umechukua hatua za kupunguza kanuni zinazodhibiti maendeleo ya AI, kwa lengo la kuharakisha ubunifu na ushindani wa kiteknolojia.

Waraka wa Papa Leo una umuhimu gani?

Wataalamu wa masuala ya teknolojia na maadili wanasema waraka huo unaweza kuchochea mjadala mpana duniani kuhusu uwajibikaji na mipaka ya matumizi ya AI, hasa katika maeneo nyeti kama usalama, vita na haki za binadamu.

Waraka wa Magnifica Humanitas unatarajiwa kuwa nyaraka muhimu kwa viongozi wa dini, serikali na sekta ya teknolojia katika kujadili mustakabali wa matumizi ya akili mnemba na athari zake kwa jamii ya kimataifa.

Kauli za Papa Leo zinakuja wakati ambapo dunia inaendelea kushuhudia maendeleo ya kasi katika teknolojia ya akili mnemba, huku makampuni makubwa na mataifa yakishindana kuongoza katika ubunifu huo. Hata hivyo, maendeleo hayo yamezua maswali mazito kuhusu maadili, uwajibikaji na usalama wa binadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *