Wetangula ataka makanisa kuhamasisha usajili wa wapiga kura

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, ameyataka makanisa kuongoza hamasisho la usajili wa wapiga kura katika eneo la Magharibi mwa Kenya.

Amesema wananchi wengi wanaostahili kupiga kura tayari wana vitambulisho vya taifa, lakini bado hawajajisajili na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC.

Akizungumza  katika hafla ya kuchangisha pesa za kusaidia kina mama katika Dayosisi ya ACK Mumias, Nangili, eneo la bunge la Matungu, Spika Wetang’ula amewahimiza viongozi wa dini na hasa kina mama kuhamasisha Wakenya wanaostahili kujisajili kama wapiga kura kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Alisema utafiti uliofanywa na viongozi wa eneo hilo unaonyesha kuwa takriban wakazi 400,000 wa Kaunti ya Kakamega na wengine 346,000 wa Kaunti ya Bungoma wana vitambulisho vya taifa lakini bado hawajajisajili kama wapiga kura.

Akinukuu msemo maarufu kwamba “viongozi wabaya huchaguliwa na watu wema ambao hawapigi kura,” Spika aliwasihi wakazi kulichukulia suala la usajili wa wapiga kura kama wajibu wa kiraia.

Wetang’ula pia aliutaka Umoja wa Kina Mama kuwa mabalozi wa usajili wa wapiga kura, akisema kuwa kaunti tano za Bungoma, Kakamega, Busia, Vihiga na Trans Nzoia zina uwezo wa kutoa zaidi ya kura milioni tano ikiwa wakazi wote wanaostahili watasajiliwa.

Spika huyo pia alitoa wito wa kuwepo kwa siasa za amani zinazojikita katika hoja, huku akiwaonya viongozi dhidi ya mashambulizi ya kibinafsi na matamshi yanayochochea migawanyiko.


Wetang’ula alitetea rekodi ya maendeleo ya Rais William Ruto katika eneo la Magharibi mwa Kenya, akisema kuwa eneo hilo limepokea uwekezaji mkubwa zaidi wa serikali kuliko ilivyokuwa chini ya tawala zilizopita.

Alitaja kufufuliwa kwa viwanda vya sukari vya Mumias na Nzoia, kuendelea tena kwa miradi iliyokuwa imesimama kama Uwanja wa Bukhungu na Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kiwango cha Sita ya Kakamega, ujenzi unaoendelea wa masoko ya kisasa katika eneo hilo, pamoja na mpango wa kuongeza Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Naivasha hadi Malaba, kama ushahidi wa dhamira ya serikali kuendeleza eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *