Askofu wa jimbo katoliki la Eldoret Dominic Kimengich amewakosoa baadhi ya viongozi wanoshinikiza kuwa mazungumzo baina ya serikali na upinzani yafanywe kwenye bunge pekee akisema kuwa mdahalo huo unastahili kujumuisha washikadau mbalimbali kwa manufaa ya wakenya wote.
Akizungumza baada ya kuongoza misa ya pasaka askofu Dominic Kimengich ameshabikia serikali ya Kenya kwanza na upinzani kukubali kushiriki meza ya mazungumzo japo ametilia shaka nia ya kuandaa mazungumzo hayo kwenye bunge akisema kuwa huenda mazungumzo hayo yakakosa kuangazia maslahi ya wakenya ambao kwa sasa wamesakamwa na hali ngumu ya kiuchumi miongoni mwa maswala mengine.
Askofu Kimengich kadhalika amekosoa mfumo wa uongozi ulioko kwenye katiba kwa sasa akisema kuwa mfumo huo ambao unampa fursa aliyeshinda kwenye uchaguzi kuongoza serikali kwa ujumla wake ndio chanzo cha mgogoro unaoshuhudiwa nchini kila baada ya uchaguzi mkuu.
Amewataka viongozi hao kukoma kutupiana cheche za maneno na badala yake kuangazia maswala yanayowakumba wakenya, akitoa wito kwa viongozi wa upinzani kukoma kutoa masharti ambayo huenda yakayumbisha mazungumzo yatakayokuwa na lengo la kuleta amani nchini.