Mwakilishi kike katika kaunti ya Uasin Gishu Gladys Boss Sholei amewahimiza wakulima katika kaunti hii kutumia mashamba yao vyema kujiinua kimaisha kupitia kilimo.
Akiongea na wanahabari katika eneo La Kapseret ,mwakilishi huyo ambaye pia ni naibu spika katika bunge la Kitaifa amesema kwamba umaskini unaoshuhudiwa miongoni mwa wakenya wengi hutokana na hulka ya kuuza mashamba kiholela holela swala analosema sharti lisitishwe na wakulima hao wafikirie mbinu mwafaka ya kupata pesa.
Kiongozi huyo vilevile alisema kwamba wakulima nchini wakijishughulisha na kilimo biashara kila mara kuanzia sasa katika miaka zijazo watakuwa watu wakutegemewa na kujitegemea katika maisha na kusaidia serikali katika uzalishaji wa chakula nchini, hii ikiwa ni njia moja ya kupunguza uagizaji wa chakula hicho kutoka katika mataifa ya nje.
Wakati huo,aliwahakikishia wakulima kaunti nzima kuwa watapokea mbolea ya Ruzuku kwa muda unaofaa, akieleza kwamba kuna njia mwafaka ambazo zinatumiwa ikizingatiwa kwamba mfumo wa kidijitali inatumiwa kwa mara ya kwanza.
Yanajiri haya wakati na ambapo kumeshuhudiwa lalama kutoka kwa wakulima katika wadi ya Kapseret/Simat na maeneo mengine kaunti nzima wakilalamikia kutopokea mbolea hiyo ya ruzuku,huku chifu wa eneo hilo akieleza kwamba hilo lilishuhudiwa kutokana na idadi ndogo ya wakulima waliojiandikisha na wengi kujitokeza kuliko wale waliosajiliwa na majina yao kunakiliwa.