Kanisa Katoliki nchini halitayafunga maeneo yake ya kuabudu kutokana na hofu ya virusi vya Corona, japo maaskfou wameagizwa kuwa makini kuepuka mikusanyiko ya watu wengi.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, kongamano la maaskofu wakatoliki nchini (KCCB), limehimiza kufanyika kwa Misa fupi na wanaohudhuria misa hizo wametakiwa kusimama umbali wa mita moja kutoka kwa mwengine.
Aidha maaskofu wameombwa kuzingatia ujumbe wa kuwapa watu matumaini na kujiepusha na mahubiri ya kuzua wasiwasi.
Wakati uo huo shughuli za kuwapa waumini Ekaristi Takatifu zitaendelea kanisani huku wanaoshughulikia sadaka wakitakiwa kuvaa vifaa vya kujikinga.
Waumini wametakiwa kuhudhuria kwa hiari misa na maombi huku wanaoslia nyumbani wakiombwa kufuatilia Misa kwenye runinga au Redioni.
Maaskofu hao wameomba vituo vya redio vinavyodhaminiwa na kanisa Katoliki kupeperusha Misa za moja kwa moja ili kuwafaidi waumini wasiohudhuria kanisani.
KCCB vilevile imesitisha Misa za Jumuiya na badala yake kuwaelekeza mapadri kufanya Misa kanisani au kwenye vituo kwa ajili ya waumini.
Kuhusu shughuli za matanga na harusi, maaskofu wamewahimiza mapadri na wakristu kufuata taratibu ambazo zimetolewa na serikali na pia kongamano hilo hasa idadi ndogo ya wanaohudhuria.
Kadhalika wametoa wito kwa wakenya na wakristu kwa ujumla kuliombea taifa hili ili Mungu aliepushie janga la Corona sambamba na waathiriwa wapate nafuu ya haraka.
Kongamano hilo la maaskofu limesema litatoa mwelekeo kuhusu sherehe za Pasaka na sakramenti za kanisa baadae.