Viongozi wa kidini wamewataka wenzao wa kisiasa kupunguza joto la kisiasa linaloshuhudiwa nchini kwa sasa, wakionya kuwa linatishia kuvuruga amani na kuwafukuza wawekezaji wanaofika nchini kwa biashara.
Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Nyeri Anthony Muheria ametoa wito kwa viongozi wa kisiasa, kutekelezea wakenya miradi ya maendeleo waliohaidi kuelekea uchaguzi mkuu uliopita, badala ya kurindima ngoma za kisiasa kila kuchao, akisema kuwa cheche za maneno kutoka kwa wanasiasa zinatishia kusambaratisha mshikamano wa kitaifa.
Askofu Muheria aliyasema hayo kwenye sherehe ya kusherehekea mwongo Moja tangu kutawadhwa kwa mtawa Irene Stephanie Nyaadha kuwa mwenyeheri kule mukurweini , ambapo ametoa wito kwa jamii kwa ujumla kuiga mfano wa mtawa huyo aliyejisadaka bila kujibakisha katika utendakazi wake kwa jamii.
