Visa vya Ulaghai wa Mpesa vyaongezeka Eldoret

Maafisa wa upelelezi wamewanasa washukiwa watano wanaohusishwa na ongezeko la biashara ya ulaghai ya Mpesa hapa jijini Eldoret na maeneo mengine nchini.

Kulingana na polisi, operesheni hiyo iliendeshwa kufuatia malalamishi mengi yaliyoripotiwa na wahudumu wa maduka ya pesa za rununu ambao pesa za kuwezesha huduma za Mpesa zimekuwa zikitoweka kwa njia ya ulaghai na kundi maarufu la uhalifu linalohudumu katika kaunti zote.

Washukiwa hao, Geoffrey Kasamani Chula, mkazi wa Munyaka hapa jijini Eldoret, Stephen Mokaya Nyangoya, mkazi wa eneo la Tiwani huko Kitale, Paul Nganga Kariuki wa Hawaii hapa Eldoret, Teresia Muthoni Mwaniki wa eneo la Kimumu hapa jijini Eldoret na Cedela Akoth Oruya kutoka Kibosi huko Kisumu walitiwa nguvuni katika oparesheni hiyo kubwa inayoendelea.

Kitengo maalum cha DCI chenye timu ya operesheni pia kilinasa gari lenye nambari ya usajili KBW 441J aina ya premio ambayo walikuwa wakiendesha ambapo laini kadhaa za simu zilizosajiliwa kwa majina tofauti na simu za rununu za aina mbalimbali zilipatikana.

Washukiwa hao wamesindikizwa hadi kituo cha polisi cha Ruai jijini Nairobi ambapo moja ya ripoti hizo iliwasilishwa, na vituo vingine vilivyo na matukio sawa na hayo vimetafutwa ili kuwachunguza zaidi washukiwa hao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *