Walimu wametakiwa kumakinikia taaluma yao licha ya changamoto ambazo zinazingira taaluma hiyo.
Akihuburi kwenye warsha iliyowaleta walimu wakuu wa shule mbalimbali za katoliki hapa nchini askofu wa jimbo katoliki la Kitui Joseph Mwongela ametoa wito kwa walimu kuwarekebisha wanafunzi wao kwa upendo akiwaonya dhidi ya kuwabagua wanafunzi kitabia.
Askofu Mwongela alisema kuwa wanafunzi wanatoka katika familia zilizo na changamoto mbalimbali na umakinifu wao ndio itakayowasaidia kuwasikiliza wanafunzi hao kuwaelekeza na hatimaye kuwa watu wakutegemewa katika jamii.
Aliwakanya walimu wakuu dhidi ya kunung’unikia sehemu za kazi akiwahimiza kuwa tayari siku zote kuhudumia jamii katika sehemu yoyote ile watakapotumwa.
Askofu Mwongela alitoa wito kwa walimu hao kujitahidi kufanya mabadiliko katika sehemu zao za kazi kwa kujenga uhusiano bora kati yao na wazazi ili shule zinazomilikiwa na kanisa katoliki ziweze kutia fora zaidi.