Maaskofu wa Kanisa Katoliki Nchini wamemhimiza Rais William Ruto kutotia saini mswada wa fedha wa mwaka 2024/2025 ili kutoa nafasi zaidi kwa ushirikishwaji wa maoni na mapendekezo kutoka kwa umma.
Wakiongozwa na mwenyekiti wa Kongamano la Maaskofu hao (KCCB), Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Kisumu Maurice Muhatia Makumba, maaskofu hao walisema maandamano ya Wakenya kupinga mswada huo ni ishara tosha kwamba hawakubaliani na mapendekezo yake.
Maaskofu hao aidha, walikashifu maafisa wa polisi na baadhi ya waandamanaji waliosababisha fujo zilizochangia maafa, majeruhi na uharibifu wa mali wakati wa maandamano hayo yaliyoshuhudiwa katika sehemu mbalimbali nchini.
Waliwataka vijana wa kizazi kipya maarufu kama Gen-Z kuzingatia sheria wanapoandamana huku pia wakiwataka viongozi kusikiliza na kushughulikia lalama zinazoibuliwa na wakenya kuhusu masuala muhimu yanayowakumba.
Vilevile Maaskofu hao waliwataka waumini wa Kanisa Katoliki kote nchini kuombea taifa la Kenya kwa kipindi cha siku tisa kupitia sala za Novena ya Moyo Mtakatifu wa Yesu.