Naibu Gavana wa Uasin Gishu mhandisi John Barorot, ametoa wito kwa uongozi wa Matatu kubadilisha sekta yao na kujihusisha na shughuli zingine za kukuza uchumi akibainisha kuwa Matatu ni biashara rasmi kama biashara nyingine yoyote na ipo haja ya kuhakikisha kwamba inaundawa upya.
Akizungumza katika makao makuu ya kaunti wakati wa mkutano na viongozi mbalimbali wa vyama vya Matatu kuhusu urekebishaji wa vituo vya kuegesha na kuabiri na ushindani wa haki, Barorot amewataka kufanya kazi kwa pamoja kama sekta kwa lengo moja akibainisha kuwa utaratibu lazima uandaliwe ili kufanikisha uchukuzi katika mji huu wa Eldoret.
Mkutano huo unajiri siku chache baada ya Gavana Bii kutangaza kupunguzwa kwa ushuru wa kila mwezi na wa kila siku unaotozwa kutoka kwa pikipiki, teksi, tuk-tuks na Matatu.
Kupunguzwa kwa ada za Matatu ni kama ifuatavyo, ada ya kuzuiliwa ilipunguzwa kutoka shilingi 26,100 hadi shilingi 5,000, ada ya kuhifadhi ilipunguzwa kutoka shilingi 3,000 kwa saa hadi shilingi 1,000 kwa siku na ada ya kizuizi ilipunguzwa kutoka shilingi 8,000 hadi shilingi 1,000.
Naye waziri wa Biashara na Ushirika katika kaunti hiyo, Martha Cheruto ameutaka uongozi wa vyama vya ushirika vya matatu kuhakikisha wanajitangaza vyema ili kurahisisha utambuzi.
Cheruto aidha, amewataka wahudumu wa matatu kufuata kanuni za trafiki za kaunti na za kitaifa ili kufanikisha utendakazi mzuri na maafisa wa kitaifa na wale wa kaunti