Seneta kaunti ya Uasin Gishu Jackson Mandago aliiomba wizara ya kilimo kuhakikisha maghala ya kutosha yanapatikana katika maeneo ya mashinani kuwarahisishia wakulima shughuli zao za uhifadhi wa mazao yao kabla ya kuzifikisha sokoni.
Akiongea na idhaa hii Mandago alisema kwamba inapasa wizara ya kilimo kuweka mikakati ya kudumu kwa kuwahusisha washikadau mbalimbali kwenye sekta hiyo hasa kwa kuruhusu vyama vya ushirika vilivyo chini ya miungano mbalimbali ya wakulima kutatua changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa njia ya karibu kwa wakulima hao.
Mandago amesema kwamba ni kupitia ushirikano huo utafanikisha kuongeza kapu la chakula la taifa hili na kupunguza uagizaji wa chakula kutoka mataifa za nje na pia kuziba pengo la uwepo wa njaa nchini.
Aidha,seneta huyo aliwashauri maafisa wa kilimo kuhakikisha wamewa elimisha ipasavyo wakulima kuhusiana na kuimarisha kilimo chao kwa kuegemea teknolojia ya kisaa akieleza kwamba hili litasaidia pakubwa kwa wakulima hao kutoegemea sana mbinu za kitambo za ukilima na kuongeza mapato yao.