maafisa mashakani

Wakaazi wa kaunti ya  Uasin Gishu na mashirika ya kutetea haki za Kibinadamu yakiendelea kulalamikia ukatili wa askari wa kaunti na maafisa wengine wa kaunti dhidi ya wafanyabiashara, waendesha bodaboda, miongoni mwa watu wengine, mahakama ya Eldoret imempata mmoja wa maafisa wakuu wa kaunti hiyo na kesi ya kujibu baada ya kushtakiwa kwa kumshambulia mfanyabiashara wa bucha wakati wa msako dhidi ya karatasi za plastiki zilizopigwa marufuku.

Hakimu mwandamizi wa Eldoret Mogire Onkoba alimpata Jeremiah Cheruiyot Kipruto, afisa wa utekelezaji sheria za kaunti katika idara ya afya ya umma na kesi ya kujibu.

Afisa huyo anadaiwa kumshambulia na kumjeruhi mfanyabiashara katika mtaa wa Kipkaren

ambapo mahakama iliambiwa kuwa mnamo Mei 15, 2019 katika mtaa wa Kipkaren katika Kaunti Ndogo ya Kapsaret mshtakiwa alimvamia Albert Chabaka Ontita muuzaji nyama alipopatikana akifunga nyama kwenye mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku.

Mahakama iliambiwa kwamba mshtakiwa ambaye alikuwa pamoja na maafisa wengine wanane wa kaunti hiyo, alimshambulia mfanyabiashara huyo kabla ya kumjeruhi vibaya mwilini.

Taarifa za kimatibabu zilizopo mahakamani zinaeleza kuwa mlalamishi alipata majeraha kadhaa kifuani na magotini baada ya mshitakiwa kudaiwa kumvamia kwa mateke na makofi.

Mahakama imeagiza upande wa utetezi kuwasilisha mawasilisho yao kwa maandishi mahakamani kwa muda wa wiki mbili zijazo.

Kesi hiyo itatajwa Agosti 25 kabla ya kutolewa kwa hukumu.

Kufikia sasa kuna zaidi ya kesi tano sawia dhidi ya maafisa wa kaunti wanaodaiwa kushambulia wafanyabiashara katika mji wa Eldoret.

Miongoni mwa visa hivyo ni kesi ya wizi wa kutumia nguvu inayomhusisha askari wa kaunti ambaye alishtakiwa kwa kutumia nguvu kumwibia mhudumu wa matatu wakati wa operesheni ya askari wa kaunti.

Kisa cha hivi punde zaidi ni kesi ambapo afisa mwandamizi wa utekelezaji wa sheria za kaunti anakabiliwa na shtaka la kutishia kumuua Hakimu mkuu Mkazi.

Kesi zote bado ziko mahakamani.

Kufuatia matukio hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha kutetea haki za kibinadamu cha Centre Against Torture Kimutai Kirui ametoa wito kwa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP kuagiza uchunguzi kuhusu visa ambapo wafanyabiashara wa Eldoret wamekuwa wakivamiwa na watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa usalama wa kaunti.

Kulingana na Kirui, zaidi ya watu 100 wameshambuliwa kinyama na kujeruhiwa na maafisa hao katika kipindi kischopungua mwaka mmoja.

Mmoja wa waathiriwa wa shambulio hilo Samson Kipchirchir Chumba ambaye ni mhudumu wa boda boda alipigwa kikatili na kuvunjwa mguu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *