Shinikizo zaidi zinazidi kutolewa kwa serikali na idara ya mahakama kubatilisha uamuzi uliotolewa na mahakama ya upeo kuwapa mashoga uhuru wa kusajiliwa na kutangamana nchini.
Viongozi wa kidini katika kaunti ya Vihiga wamelaani uamuzi huo wa mahakama wakitoa wito kwa wabunge kuunga mkono mswada unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni na mbunge wa Homabay mjini Peter Kaluma unaoharamisha hulka hiyo ya ushoga nchini.
Maimam na Wahubiri wa dini za kiislamu na wale wa kikristu kwa kauli moja wameapa kuandamana iwapo uamuzi huo hautabatilishwa, wakimtaka rais William Ruto kuvunja kimya chake kuhusu swala hili, wakitoa makataa kwa serikali na idara ya mahakama na msajili wa vyama vya ushirika kutokubali kusajili muungano huo wa mashoga almaarufu LGBTQ.
Viongozi hao sasa walitishia kulemaza shughuli za masomo nchini, wakisema kuwa sekta za elimu ikiwemo shule za msingi na sekondari pamoja na vyuo vikuu ndio sekta inayolengwa zaidi na wanaoshinikiza hulka hii.