Papa Francis amteua askofu mkuu Philip Anyolo kuwa askofu mkuu mpya wa Nairobi.

Baba Mtakatifu Francisco amemteua askofu mkuu Phillip Anyolo kuwa askofu mkuu mpya wa jimbo kuu katoliki la Nairobi.

Habari ya uteuzi wake ilitolewa rasmi huko Vatican majira ya saa sita mchana sawa na saa saba mchana za hapa nchini.

Mwakilishi wa Baba Mtakatifu nchini Kenya na Sudan Kusini Bert Van Megen, kadhalika, ametuma ujumbe huo kwa kongamano la maaskofu wakatoliki nchini (KCCB).

Askofu mkuu mteule Phillip Anyolo ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa KCCB                       kuanzia Oktoba, 2013 hadi Mei, mwaka 2021, anachukua mahala pake askofu mkuu kadinali John Njue aliyestaafu mnamo tarehe 4, Januari mwaka huu baada ya kufikisha umri wa kustaafu kwa maaskofu.

Askofu msaidizi (Auxilliary Bishop) wa jimbo kuu katoliki la Nairobi David Kamau amekuwa akihudumu kama msimamizi wa kitume (Apostolic Administrator) wa jimbo kuu la Nairobi tangu kustaafu kwa kadinali John Njue.

Askofu mkuu Phillip Anyolo ambaye sasa ni askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Kisumu, ataendelea kuhudumu hadi atakaposimikwa rasmi na kuchukua uongozi wa jimbo kuu la Nairobi.

Askofu Anyolo alizaliwa mnamo tarehe 18, Mei mwaka 1954 katika eneo la Tongaren huko Bungoma. Alipata daraja takatifu la upadri katika jimbo katoliki la Eldoret mwaka wa 1983.

Papa Yohane Paulo wa pili alimteua kuwa askofu wa jimbo katoliki la Kericho mnamo tarehe 6, Desemba mwaka wa 1995 na kutawazwa askofu tarehe 3, Februari, mwaka wa   1996.

Tarehe 20, Februari, mwaka wa 2002 Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili alimteua kuwa msimamizi wa kitume wa jimbo la Homabay kufuatia kujiuzulu kwa askofu Linus Okok Okwach.

Aliteuliwa askofu wa jimbo katoliki la Homabay tarehe 22, Machi mwaka 2003 na kusimikwa tarehe 23, Mei mwaka uo huo.

Mnamo tarehe 15, Novemba mwaka 2018, askofu mkuu Phillip Anyolo aliteuliwa kuwa askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Kisumu na kusimikwa tarehe 16, Januari mwaka 2019. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *