WAHUDUMU wa afya nchini sasa wamesitisha mgomo wao ambao ulipangiwa kuanza leo Jumatatu kwa siku 21 kwa kile walichosema ni kutoa nafasi kwa mazungumzo baina yao na serikali.
Ilani waliotoa kwa mgomo huo ilikuwa inakamilika jana Jumapili.
Wakihutubia wanahabari,Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) Seth Panyako na mwenzake wa Chama cha Maafisa wa Kliniki (Kuco) George Gibore waliongeza kuwa hatua hiyo pia imechochewa na changamoto zinazolikabili taifa hili.
Panyako aliongeza kuwa wahudumu wa afya wangesusia kazi kungetokea shida nyingi zaidi katika sekta ya afya wakati huu ambapo janga la corona limesababisha shida nyingi kwa uchumi kando na masaibu yanayosababishwa na mafuriko.
Kwa hivyo, alisema mgomo utakuwa hatua ya mwisho endapo matakwa yao hayatashughulikiwa.
Mapema Mei 2020 wahudumu wa afya walitoa ilani ya mgomo wakitaka marupurupu yao ya kufanya kazi katika mazingira hatari yasawazishwe na wapewe vifaa tosha vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona (PPE). Pia walilamika kuwa hakuna mafunzo maalum ambayo wamepewa kuhusiana na vita dhidi ya virusi vya corona huku wakitaka mazingira yao ya kufanyia kazi yaimarishwe.