Mafuriko yaleta balaa barabara tofauti nchini

Maelfu ya Wakenya sasa wamelazimika kukita kambi katika shule mbalimbali nchini kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha na kusababisha hasara kubwa.

Katika kaunti ya Nakuru, wafanyabiashara wengi walilazimika kufunga shughuli zao baada ya barabara eneo la Koinange kukatika katikati sehemu mbili na kufanya shughuli za usafiri eneo hilo kusitishwa kwa muda. Wakti huo Barabara ya kuelekea kaunti ya Bungoma kutoka eneo bunge la Mumias imefungwa ghafla baada ya maji kuvunjia kingo zake na kuvunja daraja inayounganisha maeneo hayo mawili.

Wahudumu wa bodaboda na waendeshaji wa magari sasa wametakiwa kutumia njia mbadala ili kuepukana na eneo hilo ambalo kumeshuhudiwa shimo kubwa baada ya daraja hiyo kubomoka.

Yakijiri hayo hayo katika eneo bunge la Budalangi kaunti ya Busia, baadhi ya afisi zilifurika maji kutokana na mvua kubwa inayoshuhudiwa magharibi mwa kenya, wengi wakilazimika kuhama makwao. Wakulima magharibi mwa Kenya wameelezea kupata hasara kubwa msimu huu wa upanzi baada ya mimea yao kusombwa na mafuriko hayo.

Mvua nyingi inayoendelea kunyesha nchini imesababisha hasara kubwa huku mamia ya wakenya wakipoteza maisha yao na wengine kulazimika kuhama makwao baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *