DCI yaanza Kuchunguza Kifo cha Prof Walibora

Idara ya Upelelezi ya kesi za Jinai, DCI, sasa imeanzisha uchunguzi ili kubaini iwapo Profesa Ken Walibora alifariki kutokana na ajali ya kawaida.

Duru zilisema hatua ya DCI kutaka uchunguzi wa kina zilifanya mpango wa upasuaji wa mwili wake kuahirishwa Alhamisi.

Mwili wa msomi huyo maarufu sasa umepangiwa kufanyiwa upasuaji leo alasiri katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ili kufichua alivyofariki.

Hapo jana, mwili wa Prof Walibora ulihamishwa hadi katika kitengo cha watu mashuhuri katika hifadhi ya maiti ya KNH huku familia ikishughulikia mipango ya mazishi.

Mnamo Jumatano, ilifichuka kwamba Prof Walibora aliaga dunia kutokana na majeraha mazito aliyoyapata baada ya kugongwa na basi la ‘Double M’ katika barabara ya Landhies, Nairobi karibu na kituo cha mabasi cha Machakos Country Bus.

Ilisemekana ajali ilitokea mnamo Ijumaa ya Aprili 10, 2020.

Lakini baadhi ya jamaa na marafiki zake wa karibu walitilia shaka habari hizo, baada ya gari lake jeusi aina ya Mercedes Benz kupatikana likiwa limeegeshwa kwenye barabara ya Kijabe, Nairobi, umbali wa takriban kilomita nne. Gari hilo lilikokotwa hadi katika Kituo cha Polisi cha Central katikati mwa jiji la Nairobi ambapo duru zilisema polisi wa kitengo cha DCI walitarajia kulichunguza kwa kina.

Utata kuhusu jinsi Prof Walibora alivyohusika katika ajali alipokuwa akivuka barabara kwa miguu pamoja na kufikishwa KNH alikotibiwa na kuaga dunia baadaye bila kutambuliwa na yeyote, ni kati ya mambo yaliyozua shaka miongoni mwa jamaa na wandani wake.

Inatarajiwa baada ya uchunguzi kukamilika na mwili kufanyiwa upasuaji, mazishi yataandaliwa nyumbani kwao katika kijiji cha Makutano Kwa Ngozi, eneo la Cherangany, Kaunti ya Trans-Nzoia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *