Kuvalia Maski sasa ni Lazima

Polisi wameanza kuwakamata na kuwafungulia mashtaka watu watakaopatikana katika maeneo ya umma bila maski.

Hayo yanajiri baada ya Inspekta Mkuu wa Polisi, Hillary Mutyambai, kusema kuwa hatua hiyo inatokana na idadi kubwa ya wananchi kuendelea kukiuka agizo hilo ambalo lilitolewa na serikali ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya korona.

kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mutyambai alisisistiza kwamba pana haja ya kila mwananchi kufuata maagizo ya serikali ya kukabili korona. Serikali aidha imesisitiza kwamba maski zote lazima ziafikie viwango vinavyohitajika na Wizara ya Afya ili kuzuia maambukizi ya virusi vya korona.

Msemaji wa Serikali Kanali Mustaafu Cyrus Oguna, amesema licha ya kwamba kila mmoja anastahili kuvalia maski kwenye maeneo ya umma lazima ahakikishe kuwa maski anayovalia imetengenezwa kwa ubora unaohitajika.

Oguna amesema kampuni tatu kwenye maeneo ya Nakuru, Kitui na Machakos zimepewa idhini ya kutengeneza maskini zenye ubora zitakazosambazwa kwa Wakenya.

Ikumbukwe, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe aliwaagiza wananchi wanaoyatembelea maeneo ya umma yakiwamo sokoni, na kwenye maduka makuu kuvaa maski ili kudhibiti virusi hivyo. Katika agizo hilo aidha aliagiza madereva na abiria vilevile kuhakikisha kwamba wanavaa maski wanapokuwa kwenye safari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *