Naibu wa rais William Ruto amewataka wakenya kuzingatia masharti yaliyotolewa na serikali kama vile kuvalia barakoa, kuwa umbali wa mita 1 na watu wengine na kuosha mikono na viyeyuzi ama sanitizers ambazo zimedhibitishwa na mamlaka ya kutathmini ubora wa bidhaa nchini KEBS kama njia ya kukabiliana na virusi vya Corona .
Aidha Ruto amesema serikali kwa ushirikiano na serikali za Ugatuzi wameweka mipango ya kuajiri maafisa wa afya zaidi ya 1000 wiki hii ili kushirikiana na maafisa wengine.
Ruto pia amesema magavana wa magutuzi yote 47 nchini ni sharti kutenga shule za bweni ambazo zitatumika kama maeneo ya kutenga watu watakaopatikana na virusi hivyo.
Kwa waajiri nchini, Ruto amesema umefikia wakati ambapo inastahili waajiri wote kuwaruhusu wafanyakazi wao kufanyia kazi nyumbani ili kupunguza maambukizi ya Corona. Ruto ameelezea kusikitishwa kwake na idadi kubwa ya hasara ambayo virusi vya Corona vimesababisha kutokana na idadi kubwa ya biashara na kampuni nchini na hata ulimwenguni kusitisha shughuli zake.
Naibu wa rais pia ameyataka makanisa na viongozi wake kuliweka taifa la Kenya kwa maombi wakati huu ambapo idadi kubwa ya maambukizi yanaendelea kushuhudiwa nchini. Ameongeza kuwa serikali imetathmimi idadi ya watu wenye mahitaji spesheli kwa jamii na sasa serikali itaanza kugharamia mahitaji yao muhimu kama chakula, matibabu na vitu vingine