Mwakilishi
wa Wadi ya Kapchemutwa katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet Ambrose Kiplagat
na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika riadha Wilson Kipsang, wamekesha
korokoroni baada ya kukamatwa na maafisa wa polisi kwa tuhuma za
kukiuka amri ya kutopatikana nje kati ya saa moja usiku na saa kumi na
moja alfajiri.
Wawili hao pamoja na wengine zaidi ya kumi
walikamatwa Alhamisi wakinywa pombe kwenye eneo moja la burudani
mjini Iten mwendo wa saa mbili usiku. Kabla ya kukamtwa kwao, kundi hilo
lilizua vurugu likinga kukamatwa huku polisi wakilazimika kuwaita
maafisa zaidi kuwasaidia kuwakabili.
Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Elgeyo
Marakwet John Mwinzi amesema kuwa walipokea ripoti kutoka kwa umma kuhusu
washukiwa waliokuwa wamejifungia kwenye eneo moja la burudani.
Mwinzi hata hivyo, amewaomba Wakenya kuendelea kufuata maagizo ya
serikali ya kuzuia maambukizi ya virusi vya korona.
Wote waliokamatwa wanazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Iten wakitarajiwa
kushtakiwa Ijumaa.