Huenda kila Mkenya akalazimika kutumia barakoa za uso, yaani face masks kujikinga kutokana na maambukizi au kusambaza virusi vya korona, iwapo Shirika la Afya Duniani WHO litaidhinisha mapendekezo mapya kuhusu namna ya kukabili virusi hivyo hatari.
Huku tafiti mbalimbali zikiendelea kuonesha kwamba huenda virusi vya korona vinasambaa pia kupitia hewa, WHO inalenga kubadili msimamo wake wa awali kwamba ni wahudumu wa afya pekee, walioambukizwa au wanaowachunga wagonjwa ndio wanaostahili kuvaa barakoa.
Baadhi ya mikakati ya shirika hilo ya kukabili maambukizi ni kunawa mikono, kuzingatia usafi wa hali ya juu na kujiepusha na maeneo yaliyo na watu wengi.
Hayo yanajiri huku serikali ikitoa agizo kwa wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma, tuktuk pamoja na abiria wao kutumia barakoa kuzuia maambukizi zaidi kufuatia kuongezeka kwa virusi hivyo humu nchini. Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema hatua hiyo ni miongoni mwa mikakati zaidi inayowekwa na serikali kuzuia kusambaa kwa korona akisema ina mpango wa kuanza kutengeneza barakoa zitakazosambazwa kwa umma.
Kwa mara nyingine, Waziri huyo amewashauri Wakenya kujiepusha na safari za mara kwa mara iwapo hakuna dharura hasa kwa wakazi wa Nairobi kujiepusha kueleka maeneo ya mashambani.
Ili kuhakikisha kwamba sekta ya afya inajiandaa vilivyo kukabili idadi kubwa ya maambukizi iwapo visa zaidi vitaripotiwa, Kagwe amesema jumla ya Wahudumu wa afya elfu sita wataajiriwa katika kipindi cha siku saba zijazo huku serikali za kaunti zikiagizwa kuanza shughuli hiyo mara moja.
Miongoni mwa elfu sita hao, elfu moja wataajiriwa kwenye kwenye hospitali za Level 4, 5, 6, Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na ile ya Mafunzo ya Rufaa ya Kenyatta, shughuli ambayo vile vile inatarajiwa kukamilika katika kipindi cha wiki moja pekee.
Tayari shule za upili kadhaa za malazi zitakazotumika kuwa vituo vya karantini zimetambuliwa huku wafanyakazi hasa wanaotengeneza vyakula wakishauriwa kujiandaa.
Kufikia sasa, watu watatu wamefariki dunia humu nchini kufuatia maambukizi ya korona huku wanaougua wakifikia mia moja na kumi na wengine wanne wamethibitishwa kupona.
Ikumbukwe serikali mapema wiki hii ilionya kwamba huenda jumla ya visa elfu kumi vikaripotiwa ifikiapo mwisho wa mwezi huu iwapo Wakenya hawatatii ushauri unaotolewa na serikali.