Wabunge wa Chama cha Amani National Congress, ANC wanatarajiwa kukutana kujadili madai ya kuwapo njama ya kumbandua mamlakani Naibu wa Rais, William Ruto.
Naibu Mwenyekiti wa ANC, Ayub Savula ambaye pia ni Mbunge wa Lugari amethibitisha kuwapo kwa mkutano huo katika hoteli moja hapa Nairobi na ambao utahudhuriwa na Mwenyekiti wao, Musalia Mudavadi pamoja na wabunge wote waliochaguliwa kupitia tiketi ya ANC. Aidha, Saluva amesema mkutano huo umechochewa na madai ya kuwapo njama ya kumbandua Rais Uhuru Kenyatta madarakani, suala linalodaiwa kujadiliwa kwa kina wakati wa mkutano wa baadhi ya wabunge wa Jubilee waliokutana mjini Naivasha wiki moja iliyopita, ulioongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Seneti, Kipchumba Murkomen. Wanasiasa wanaomuunga mkono Raila Odinga walidai kwamba wabunge hao ambao ni wafuasi wa Ruto walitumia mkutano wa Naivasha kujadili namna ya kuwasilisha bungeni hoja ya kutokuwa na imani na Rais Kenyatta.