Shule ya Upili ya wasichana ya Eregi kaunti ya Kakamega imefungwa kwa muda usiojulikana.
Hii ni baada ya wanafunzi tisini na wawili wa shule hio kulazwa katika hospitali tofauti kwenye kaunti ya Kakamega kutokana na ugonjwa ambao kufikia sasa haujadhibitishwa.
Shule hio imefungwa kutokana na uamuzi kutokana na maafikiano baina ya maafisa wa elimu kwenye serikali kuu na maafisa wakuu kwenye kaunti ya Kakamega pamoja na bodi kuu ya shule hio kuwaruhusu wanafunzi wa kidato cha kwanza,cha pili na tatu kuelekea nyumbani huku wale wa kidato cha nne wakibaki kutokana na kukaribia kwa mtihani wao wa kitaifa.
Akizungumza baada ya kuizuru shule hio,mjumbe wa kamati kuu ya elimu Sayansi na Teknolojia kaunti ya Kakamega Dr.Bonface Okoth,amesema kuwa serikali ya kaunti ya Kakamega inajitahidi ili kupata suluhu kutokana na changamoto hio ya afya inayoikumba shule hio.
Hata hivyo Okoth amesema kuwa sampuli za chembechembe za damu ya wanafunzi walioathirika zimepelekwa kwenye kituo kikuu cha utafiti wa matibabu (KEMRI) Nairobi na Kisumu ili kubaini chanzo cha ugonjwa huo.
Hata hivyo waziri wa elimu Ezekiel Machogu anatarajiwa kuzuru shule hio wakati wowote kwanzia sasa.