Viongozi wa dini la kiislamu ukanda wa kaskazini mwa bonde la ufa wametoa wito kwa umma kutochukulia visivyo uamuzi wa rais William Ruto wa kuondoa marufuku ya takriban miaka sita ya kukata miti.
Katika kikao na wana habari mjini Eldoret viongozi wa dini ya kiislamu wakiongozwa na sheikh Abubakar Bini, wamewaonya wakenya dhidi ya kuharibu misitu licha ya uamuzi huo uliotolewa mwishoni mwa juma lililopita na rais William Ruto wakitaka Shirika la Huduma ya Misitu ya Kenya (KFS) kujitokeza kuhamasisha jamii kuhusu athari za kuharibu misitu nchini.
Viongozi hao kadhalika walikariri haja ya kupiga jeki juhudi za rais William Ruto ya kutaka wakenya kujitokeza na kupanda miti kwa wingi, kama njia moja ya kukabiliana na athari za tabianchi wakitoa wito kwa kila mkenya kujizatizi na kulinda misitu dhidi ya maharamu ambao huenda wakatumia fursa hiyo kuharibu misitu kwa faida yao ya kibinafsi.
Ikumbukwe kuwa KFS ilijitokeza hapo jana na kutetea uamuzi wa raiswa kuondoa marufuku ya takriban miaka sita ya kukata miti licha ya wasiwasi ulioibuliwa na wanaharakati wa mazingira.
Shirika hilo lilieleza bayana kuwa kuondolewa kwa marufuku ya ukataji miti katika misitu nchini kulitokana na uchunguzi ulioidhinishwa na waziri wa awali wa masuala ya mazingira na misitu.
Kulingana na KFS, uchunguzi huo ulifichua idadi kubwa ya mashamba ya misitu iliyokomaa na kupitisha ata ukomavu huo hivyo kuilazimu serikali kuingililia kati na kuweza kukata miti iliyo pitisha ukomavu wake na kuoza misituni.