Mwanafunzi mmoja kutoka familia isiyojiweza katika eneo la munyaka Eldoret ana kila sababu ya kutabasamu baada ya walimu na wanafunzi wa shule ya upili ya Paul Boit katika kaunti ya Uasin Gishu kumchangia fedha za kumsaidia kujiunga na kidato cha kwanza katika shule hiyo.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Shem Busolo alisema kwamba walimhurumia mwanafunzi huyo ambaye alikua ameitwa kujiunga na shule hiyo kufika shuleni humo wakiwa na mzazi wake akiwa amejihami na barua ya kuitwa shuleni pekee bila ya kitu kingine ndiposa wakachukua hatua ya kumchangia ili aweze kupata sare za shule na vitu vingine vya kimsingi.
Kwa upande wake mwanafunzi huyo Job Kamiti alidhihirisha furaha yake akisema ni fursa sasa kutimiza ndoto yake ya kuwa rubani ingawaje ametoa wito kwa wahisani kujitokeza kumsaidia ili aweze kukamilisha masomo yake.
Naye Salina Njeri ambaye ni mamake kamiti akiweka bayana kwamba hana uwezo wa kumlipia karo mwanawe na pia akatoa wito kwa wahisani waweze kumsaidia kwani anasema biashara ya kuuza mboga imerudi chini sana hivyo Hana uwezo wowote wa kumsaidia mwanae.