Askofu wa Jimbo katoliki la Eldoret Dominic Kimengich amewaonya wakenya dhidi ya kuwabagua wenzao kwa msingi wa kikabila na badala yake kuishi kwa amani na utangamano kwa faida ya mshikamano wa kitaifa.
Katika ujumbe wake Jumapili kwa niaba ya baraza la maaskofu wa katoliki nchini KCCB kwenye parokia ya Nerkwo, askofu Kimengich alitoa wito kwa jamii kuishi kwa pamoja na kuwapuuza viongozi wanaochochea umma kuwabagua wenzao kwa misingi ya kikabila kuelekea uchaguzi mkuu wa agosti tisa mwaka huu, akitoa wito kwa kila mkenya kumkubatia mwenzake bila kujali kabila au rangi kwa manufaa ya mshikamano wa kitaifa.
Askofu kimengich kadhalika aliwataka vijana kutokubali kutumiwa na wanaisasa kuzua vurugu kabla wakati na hata baada ya uchaguzi akisema kuwa vijana nguzo muhimu kwa ukuaji wa taifa hili na kuwataka wananchi kuwa macho dhidi ya viongozi wanawatumia vijana kubuni magenge ya wahalifu kwa lengo la kuzua vurugu na kujinufaisha kisiasa.