Serikali imetoa tahadhari kutokana na hatari ya kuzuka kwa mkurupuko wa magonjwa katika mtaa wa Kihoto kwa sababu ya mafuriko yaliyozingira nyumba kadhaa kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha maji katika ziwa Naivasha.
Familia zote ambazo nyumba zao ziko ndani ya maji zimepewa wiki moja pekee kuhamia maeneo salama.
Wakati kamishna wa kanda ya Rift Valley George Natembea alipotembelea eneo la Kihoto na kushuhudia kiwango cha mafuriko alisema kwamba hali katika eneo hilo ni hatari. Alisema mipango ilikuwa inaendelea kuzisaidia familia ambazo zimeathirika kwa chakula na vifaa vinginevyo.
Mamia ya wakaazi wameathirika sana kutokana na kuongezeka kwa viwango vya maji katika maziwa katika maeneo hayo hasa katika eneo la Bonde la Ufa. Watu kadhaa wamelazimika kuhama makwao baada ya ziwa Baringo pia kufurika.
