Wetang’ula angali kiongozi wa Ford-Kenya

Jopo la kuamua mizozo ya vyama vya kisiasa Ijumaa limetamatisha kesi kuhusu mzozo wa uongozi wa chama cha Ford-Kenya huku Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula akisalia kuwa mwenyekiti wake.

Wanachama wa jopo hilo Desma Nungo, Milly Lwanga na Dkt Adelaide Mbithi wameamuru mzozo huo wa uongozi kati ya Seneta Moses Wetang’ula na Mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi utatutiliwe na chama hicho.

Punde tu baada ya jopo hilo kutamatisha kesi hiyo, mawakili Ben Millimo, Nelson Havi, Eunice Lumallas na Dkt John Khaminwa wamesema kundi linaloongozwa na Mbunge wa Kimilili Wafula Wamunyinyi litafika mbele ya kamati ya nidhamu ya chama hicho Jumanne.

Akiwasilisha ombi la kutamatisha kesi iliyoshtakiwa na Ford-Kenya kupitia kwa Lumallas, wakili mwenye tajriba ya juu Dkt Khaminwa alisema  pande zote zimekubaliana na zitafute suluhu kulingana na sheria za chama hicho.

Dkt Khaminwa walijadiliana na wakili Bryan Khaemba, wakili wa Dkt David Eseli Simiyu na Wamunyinyi na wakakubaliana kesi hiyo iondolewe kortini kisha waisuluhishe kwa mujibu wa Katiba ya chama cha Ford-K. Wakili huyo amesema waliwasilisha pendekezo lao kwa afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (RPP) Ann Nderitu ambaye hakulipinga.

Uongozi wa Ford-K kupitia kwa Wetang’ula ulipinga mapinduzi yaliyoongozwa na baadhi ya maafisa wakuu wa chama hicho.

Kundi linaloongozwa na Wamunyinyi lilichapishwa katika Gazeti rasmi la Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *