Wakazi wanaoishi katika maeneo hatari ya nyanda za chini katika Kaunti ya Pokot Magharibi wameshauriwa kuhama kutoka maeneo hatari ili kuzuia maafa ya maporomoko ya ardhi yanayoletwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo hilo.
Hii ni baada ya watu 14 kufariki, wengine kupotea na huku wengine wakijeruhiwa vibaya pamoja na mali kuharibiwa kwenye mkasa wa maporomoko ya ardhi yaliotokea katika kijiji cha Chesegon, eneo bunge la Sigor baada ya mvua kubwa kunyesha usiku wa Jumamosi.
Maeneo mengi kama vile Sondany, Tapach, Batei, Kerelwa, Muino na Seker ni ya vituo vya miinuko ya milima ambapo ni hatari huku tukio la hivi maajuzi likiwa la Chesegon ambapo watu wa kijiji hicho walipoteza makao na mali kuharibika kufuatia mvua kubwa inayonyesha eneo hilo.
Kuumekuwa na ripoti nyingi za maporomoko huku wakazi wakiombwa kuondoka katika maeneo hayo. Barabara za eneo la Muino hazipitiki baada ya kuvurugwa na mvua kubwa inayonyesha. Akiongea katika eneo la Chesegon, Mbunge wa Sigor, Peter Lochakapong aliwataka wakazi kuondoka mara moja katika nyanda za chini na kuhamia maeneo salama ili kuzuia maafa ambayo yanaweza kusababishwa na mvua hiyo.