Mwanaharakati wa haki za binadamu Okiya Omtata amesema serikali inapaswa kurejesha hela zilizolipwa na Wakenya katika vituo vya karantini kote nchini.
Omtata alisema serikali inakiuka katiba kwa kuwashurutisha Wakenya kugharamia chakula na malazi wakati wanapokuwa karantini. Kwenye kesi aliyowasilisha mahakamani Alhamisi, Aprili 23, mwanaharakati huyo alitaka korti kuamuru serikali ya Jubilee kuwalipia gharama wale wote walioko vituo vya karantini kulingana na sheria ya afya ya umma.
Alisema pia serikali inakosa kuongeza muda wale wote ambao wanazuiliwa katika vituo hivyo. Mwanaharakati huyo alisema Waziri wa Afya Mutahi Kagwe anatumia mamlaka kupita kiasi kuunda mikakati inayotumiwa kuwaadhibu wanaopatkana na makosa ilhali hilo ni jukumu la Bunge. Haya yanajiri siku chache baada ya Wizara ya Afya kuonya kwmaba wale wote ambao watanaswa wakikiuka agizo la kafyu watasukumwa karantini ya lazima na watagharamia chakula na malazi katika vituo hivyo.