Idadi ya Walioambukizwa COVID-19 Yafikia 158 Nchini Kenya

Jumla ya watu mia moja hamsini na wanane nchini wameambukizwa virusi vya korona baada ya watu kumi na sita zaidi kuthibitishwa kuambukizwa virusi hivyo hatari vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Akilihutubia taifa kuhusu mikakati ya ziada ya kukabili kusambaa kwa virusi vya korona, Rais Kenyatta amesema maafisa wa afya waliwapima watu elfu nne, mia mbili na sabini na saba katika kipindi cha saa ishirini na nne zilizopita.

Katika kikao hicho, Kenyatta aidha amesema kuwa asilimia themanini na mbili ya visa vya maambukizi vimeripotiwa katika Kaunti ya Nairobi huku asilimia kumi na nne ya jumla ya visa hivyo, vikiwa kwenye Kaunti za Kilifi, Kwale na Mombasa.

Amesema kutokana na kuendelea kuongezeka kwa maambukizi, pana haja ya Wakenya sasa kuwa makini hata zaidi na kufuata maagizo yanayotolewa na serikali ili kukabili maambukizi zaidi.

Wakati uo huo, Kenyatta amesema ni visa vichache vya mambukizi ambavyo vinawahusisha wakazi wa maeneo mengine, ambao wamekuwa wakisafiri kwenye Kaunti za Kilifi, Mombasa, Kwale vilevile Nairobi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *