Bi kizee wa miaka 62 ambaye amekuwa akishiriki ujambazi kwa miaka mingi, amefungwa jela miaka 35 baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa kimabavu.
Joyce Wairimu Kariuki alipatikana na hatia ya wizi wa mabavu uliohusisha visa vya unyang’anyi wa magari hasa malori yanayobeba mizigo maeneo ya Nakuru, Mombasa na Nairobi.
Mwanamke huyo ambaye wapelelezi wamemtaja kama kiongozi wa mtandao wa genge la majambazi, alishtakiwa Aprili 23 2019 katika Mahakama ya Loitoktok miezi michache baada ya kuachiliwa kutoka gereza la Shimo la Tewa mjini Mombasa ambako alitumikia kifungo cha miaka 15 na miezi sita kwa kesi nyingine sita za wizi alizotenda maeneo tofuati.
Kushtakiwa kwake Loitoktok kulifuatia uchunguzi ambao ulimhusisha na visa kadhaa vya watu kunyang’anywa magari kaunti za Nakuru, Nairobi na Mombasa kati ya 2018 na Aprili 2019, kumaanisha hakurekebisha tabia licha ya kufungwa jela zaidi ya miaka 15 kwa kesi za awali.
Rekodi za mahakama zinaonyesha kwamba mwanamke huyo alifungwa jela kuanzia mwaka wa 2006 baada ya kuhusika na visa vya wizi kaunti za Kilifi, Kwale, Nyeri, Murang’a, Nyahururu na Mombasa.