Elgeiyo Marakwet: Gavana Rotich azindua mpango wa KISIP

Gavana wa kaunti ya Elgeyo Marakwet Wesley Rotich amezindua mpango wa uboreshaji wa miundombinu kwa vituo vya Cheptongei na Chebiemit katika Kaunti Ndogo ya Marakwek Magharibi inayolenga kuboresha hadhi ya vituo hivyo viwili.

Akizungumza alipokuwa akiongoza hafla ya uzinduzi na uwekaji msingi wa mradi huo chini ya mpango wa Kitaifa wa Uboreshaji wa Makazi ya mabanda nchini (KISIP2) huko Cheptongei, Gavana Rotich alisema ujenzi wa miundombinu wa kima cha shilingi milioni 350, unahusisha ujenzi wa barabara za lami katika vituo hivyo viwili, kuweka taa za mlingoti wa juu, taa za barabarani,  kujenga mifumo ya mifereji ya maji, njia za kutembea na masoko.

Gavana huyo alibainisha kuwa sehemu zingine za makazi ya mabanda ikiwa ni pamoja na Kambi Debe na Milimani katika Manispaa ya Iten, pia yanatarajiwa kufaidika na mpango huo.

Aliongeza kuwa kaunti itaendelea kutafuta ushirikiano ili kuendeleza na kuboresha zaidi miji yake.

Mwakilishi wa wadi ya Moiben-Kuserwo, Hillary Kiplagat, alitoa shukrani zake kwa mradi huo, akisisitiza matokeo yake chanya kwa jamii ya eneo hilo.

Kiplagat amewataka wakazi kushirikiana na mwanakandarasi, kuhakikisha kunakuwepo na mazingira mazuri ya utekelezaji wa mradi huo.

Mradi huo unatarajiwa kuchukua miaka miwili hadi mitatu, huku vituo vingine kote kaunti hiyo vikizingatiwa katika awamu zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *