Serikali ya kaunti ya Uasin Gishu chini ya gavana Jonathan Bii Chelilim, imepiga hatua katika utekelezaji wa ajenda ya maendelo katika sekta zote za uchumi maarufu kama “Nguzo Kumi”.
Akitoa hotuba yake katika bunge la kaunti hiyo, gavana Chelilim ameelezea maendeleo yaliyoafikiwa na utawala wake katika kipindi cha mwaka mmoja katika sekta mbalimbali ikiwemo kuimarishwa kwa miundomsingi.
Kuhusu miradi ya maji, gavana Chelilim amesema serikali yake imetekeleza zaidi ya miradi 50 ya kusambaza maji katika maeneo mbalimbali ya kaunti miongoni mwa mikakati mingine inayoendelea ili kuhakikisha kuwa wakazi wanapata maji ya kutosha.
Kuhusu mikakati ya kuhifadhi mazingira na kukabili mabadiliko ya tabianchi, gavana huyo amedokeza kuwa utawala wake unapania kupanda miche milioni 15 katika kaunti nzima akiwasihi wakazi kukumbatia juhudi hizo.