Himizo limetolewa kwa wakristu kujiweka tayari kuingia katika ufalme wa mbinguni kwa kuyanyosha mapito yao.
Askofu msaidizi wa jimbo kuu katoliki la Nairobi David Kamau akizungumza wakati wa ibada ya wafu ya mtawa Merilyne Nanjala katika kanisa la Mtakatifu Austin Msongari,aliwashauri wakristu kuhakikisha wanaimarisha imani yao kwa kristu kwa kuyatenda yanayostahili maana wakishaondoka humu duniani ni vigumu kurekebisha yale wangeyanyosha wakiwa ulimwenguni.
Aliwakumbusha kwamba kuumbwa kwa mwanadamu na uwepo wake duniani kuna sababu kuu na ni kwa kila mmoja kuyatelekeza yale wanayopaswa kutimiza ndipo wajiweke tayari katika kumwona kristu.
Askofu Kamau vilevile aliwashauri wakristu kutekeleza jukumu lao kikamilifu kwa kuheshimu amri za kristu kwa njia inayostahili ndipo wanadamu wengine wapate kumfahamu mwenyezi mungu na kuwajengea maisha bora wengine wa uridhi wa ufalme wa mbingu.