Idara ya Utabiri wa hali ya hewa nchini, imesema mvua inatarajiwa kuendelea katika maeneo ya Nyanda za Juu za Kati, Bonde la Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Pwani, na Magharibi mwa Kenya.
Katika utabiri wake wa hivi punde kuanzia Mei 27 hadi Juni 2, idara hiyo imesema usambazaji wa mvua utakuwa tofauti na kiwango cha ukanda wa pwani kinachofunika Lamu na Garsen kuanzia milimita 10 hadi milimita 20.
Maeneo ya Kilifi yanayopakana na Bahari ya Hindi pia yatapata mvua ingawa ya kiasi kidogo cha kati ya milimita 1-10mm sawa na maeneo karibu na Tsavo, Bura na Kwale.
Kulingana na utabiri huo, mvua itanyesha zaidi katika eneo la Bonde la Ufa katika kaunti za Trans Nzoia, Bungoma, Uasin Gishu, Bomet, Kericho na Nakuru yenye nguvu kati ya milimita 10-20mm.
Kiwango hicho kitaongezeka hadi kati ya milimita 20-50mm katika Bonde la Ziwa Victoria na mikoa ya Magharibi mwa Kenya katika kaunti za Busia, Migori, Nyamira, Kisii, Homa Bay, Siaya, Kisumu na Vihiga.
Hali hii itaigwa katika Nyanda za Juu za Kati katika kaunti za Kiambu, Murang’a, Nyeri, Nyandarua, Tharaka Nithi, Meru na Laikipia huku kaunti za Tharaka Nithi, Nyandarua na Murang’a zikipokea hadi 120mm ya mvua.
Maeneo ndani ya Kakamega, Busia na mpaka kati ya kaunti za Nandi na Kericho pia yatapata mvua ya hadi milimita 120 huku Narok, Baringo na Elgeyo Marakwet zikisalia kavu katika kipindi chote cha utabiri.
Kaunti ya Mandera itapokea hadi 10mm za mvua, sawa na kaunti za Kajiado na Nairobi.