Gavana wa kaunti ya Elgeiyo Marakwet Wesley Rotich ametoa wito kwa familia nzima ya kanisa katoliki jimbo la Eldoret na wenyeji wa eneo la kaskazini mwa bonde la ufa kutoishutumu jamii nzima ya Marakwet kufuatia mauaji ya padre Allois Cheruiyot Bett eneo la Tot kaunti hiyo wiki jana.
Akiongea wakati wa Misa ya wafu ya mwendazake Padre Allois katika Kanisa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kathedrali hapa jijini Eldoret, gavana Rotich ameelezea kuhuzunishwa kwake na mauaji ya padre huyo akisema yamemkosesha amani kwa kuwa alimuenzi.
Wakati uo huo gavana huyo amedokeza kuwa tayari wameshauriana na wenyeji wa kaunti hiyo ambao wameahidi kuwa wahusika wa mauaji hayo watatambuliwa ndani ya siku tatu huku pia akitoa wito kwa kanisa kuendelea kuombea amani katika bonde la Kerio.
Naye gavana wa Nandi Stephen Sang’ amewataka wenyeji wa bonde la Kerio kutowaficha majangili na badala yake kushirikiana na serikali kuwatambua wahusika wa visa vya uhalifu na mauaji ili eneo hilo lipige hatua kimaendeleo.