Askofu wa jimbo Katoliki la Eldoret Dominic Kimengich amekariri wito wake kwa vyombo vya usalama kuhakikisha kwamba wahusika wa mauaji ya Padre Allois Cheruiyot Bett wametambuliwa, kukamatwa na kushtakiwa ili haki itendeke.
Kwenye homilia yake wakati wa Misa ya wafu kwa ajili ya mwendazake Padre Allois katika kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu Kathedrali hapa jijini Eldoret, askofu Kimengich amelaani vikali mauaji hayo akiitaka idara ya usalama kuwajibika.
Kwa upande wake askofu wa Kiangilikana Dayosisi ya Eldoret Christopher Rutto akiwasilisha rambiambi zake, amemtaja marehemu Padre Allois kama aliyejitolea katika utume wake licha ya kufahamu changamoto za usalama zinazolikumba eneo la Bonde la Kerio.
Padre Allois Cheruiyot aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Alhamisi wiki jana eneo la Tot kaunti ya Elgeyo Marakwet baada ya kuadhimisha Misa ya Jumuiya eneo hilo mchana.
Mwili wa padre Allois Bett utaondolewa katika makafani ya hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi hapa jijini Eldoret mnamo Jumatatu tarehe 2, Juni mwaka huu.
Umma utaruhusiwa kuutazama mwili na kutoa heshima zao mwisho kuanzia saa nane mchana kabla ya Misa ya Wafu mwendo wa saa tisa alasiri katika kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu Kathedrali.
Mwendazake atapumzishwa Jumanne Juni 3, mwaka huu katika Parokia ya Holy Family Ol’lessos eneo la Kipastorali la Nandi.
