Bunge la kaunti ya Nandi limesalia mahame kwa siku sita sasa kufuatia uharibifu uliofanyika bungeni humo baada ya vurugu kutokea wakati wa kupigia kura ripoti ya kamati maalum iliyoangazia utendakazi wa serikali ya kaunti hiyo wiki iliyopita.
Spika wa bunge la kaunti hiyo Philemon Cheruiyot alitangaza kusimamisha shughuli zote za bunge hadi mawasiliano rasmi yatakapotolewa akisema kwamba kando na uharibifu ulioshuhudiwa ndani ya bunge hilo, baadhi ya waakilishi wadi walijeruhiwa na wamekuwa wakiendelea kutibiwa.
Haya yakijiri, seneta wa Nandi Samson Cherargei amewataka waakilishi wadi kurejea bungeni ili kuendeleza shughuli za kuangazia ripoti ya kamati hiyo na kutoa matokeo kwa umma.
Cherargei amedai kuwa wawakilishi wadi hawana sababu ya kukosa vikao vya bunge akisema hata bunge la kitaifa liliendeleza vikao vyake licha ya vijana wa Gen-Z kulivamia wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024/2025.
