Askofu wa jimbo Katoliki la Eldoret Dominic Kimengich amewataka wajumbe wa Sinodi kujitolea kikamilifu katika kufanikisha malengo ya jimbo.
Akiongea wakati wa Misa ya kufungua rasmi mkutano wa wajumbe wa sinodi katika kituo cha kipastorali cha Mtakatifu Yohane Mbatizaji viungani mwa mji Eldoret Askofu Kimengich alisema ni fahari kwa wajumbe hao kushiriki katika mchakato huo ikizingatiwa kuwa ni mara ya kwanza kwa Jimbo kuzindua Sinodi tangu kubuniwa kwake.
Askofu Kimengich amesisitiza umuhimu wa Sinodi ya Jimbo akisema kutokana na mashauriano ya wajumbe hao, masuala muhimu yatatambuliwa na kupewa kipaumbele katika kuliendeleza jimbo.
Aidha alidokeza kuwa sinodi haihusishi tu mapadre au wakleri pekee bali bia inawapa nafasi wakristu walei kushiriki kikamilifu katika mchakato huo kwa manufaa ya kila mmoja jimboni.
Aliwahimiza wajumbe hao kuwa huru kutoa maoni na mchango wao kuhusu Sinodi kwani wamewezeshwa na nguvu ya Roho Mtakatifu.