Rais Uhuru Kenyatta ameionya serikali ya Somalia kuacha uchokozi wa mara kwa mara dhidi ya Kenya.
Onyo lake linajiri siku moja baada ya wakazi wa Mandera kulazimishwa kutoroka makazi yao baada ya ghasia zilizozuka kati ya wanajeshi wa Somalia dhidi ya wanajeshi wa eneo la Jubaland katika eneo la Bulla Hawa.
Wabunge kutoka mji wa Mandera wakiongea na vyombo vya habari siku ya Jumatatu kwamba mashambulizi hayo yalikuwa mabaya hali iliyowafanya wakazi kukimbilia maisha yao . Rais Uhuru amesema kwamba taifa la Somalia linapaswa kuangazia maswala ya raia wake kwa kukabiliana na kuushinda ugaidi ili kuweka amani, usalama na udhibiti katika eneo zima la Afrika mashariki.
Akiongezea kwamba Kenya haitakubali kutumika kama sababu ya changamoto zinazoikumba Somalia kisiasa.
Kiongozi huyo ametoa wito kwa Somalia kuacha kampeni hiyo chafu dhidi ya Kenya na badala yake kupeleka nguvu yake katika kutoa uongozi bora kwa watu wake.
Alisema kwamba Kenya imelazimika kuathirika pakubwa kutokana na hatua yake ya kuendelea kutoa mchango mkubwa katika kuweka amani na usalama katika nchi jirani ya Somalia. Kiongozi huyo pia amesema kwamba Kenya sasa inaunga mkono wito unaotolewa na Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa kieneo na kimataifa wanaoitaka Somalia kutafuta makubaliano mapana ya kisiasa.