BARAZA la Maspika wa Kaunti (CAF) linataka mawaziri kuwa na manaibu wao ambao si wabunge na si wanasiasa.Pia linataka mabunge ya kaunti kuwa na hazina maalum kama Bunge la Kitaifa.
Likitoa mapendekezo yake Ijumaa, limetaka wadi kuwa na hazina yake maalum ya maendeleo.Miongoni mwa mapendekezo mengine linataka Idara ya Mahakama kutengewa angalau asilimia mbili ya bajeti ya taifa, uhuru wa idara hiyo kuongezwa, miungano ya kimaendeleo ya kaunti kupewa nguvu na kufadhiliwa na Serikali ya Kitaifa huku likipinga pendekezo la kubuniwa kwa serikali za kikanda.
CAF pia inataka Baraza la Magavana (CoG) kupewa mamlaka na kujumuishwa kikatiba, IEBC ibaki ilivyo; kusiwe na mwingilio wa kisiasa na vilevile kugatuliwa kwa utendakazi wa IEBC kiasi kwamba matokeo ya magavana, maseneta, wabunge wa maeneobunge ya kaunti kutangazwa katika kaunti. Pia kuna pendekezo kwamba uchaguzi wa nyadhifa zote uwe ukifanywa siku moja na IEBC isifanyiwe mageuzi yoyote miaka miwili baada ya uchaguzi.