Polisi wameanzisha msako wa kuwatafuta wazazi wa mtoto wa miaka 2 aliyefariki baada ya kuripotiwa kuangukia kwenye kontena lililojazwa pombe haramu katika Kaunti ya Pokot Magharibi.
Kulingana na maafisa wa polisi ambao wanachunguza, kisa hicho kilichotokea eneo la Kaisagat katika Wadi ya Siyoi wamewalaumu wazazi kwa kuzembea katika malezi yao kwa wanao.
Maafisa wa Kituo cha Polisi cha Kapenguria waliitikia wito wa majirani na kukimbilia eneo la tukio.
Kamanda wa polisi wa Kapenguria Kipkemoi Kirui alisema pombe hiyo mbichi, almaarufu kangara, iliripotiwa kufichwa katika shamba la familia hiyo.
Pombe mbichi, ambayo hatimaye ingetumika kutengenezea chang’aa, ilikuwa imezikwa kwenye vyombo.
Wazazi hao ambao awali walidai kuwa mtoto wao mwenye umri wa miaka 2 alizama kwenye beseni la maji, wamejificha.
Wananchi wametakiwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia katika uchunguzi.