Serikali imetangaza Jumanne, Februari 11, 2020, kuwa siku ya mapumziko kuwapa Wakenya nafasi kuomboleza Rais Mstaafu Daniel Arap Moi aliyefariki Jumanne ya Februari 4, katika Nairobi Hospital.
Tayari Waziri wa Masuala ya Ndani ya nchi, Dkt. Fred Matiang’i amechapisha katika Gazeti Rasmi la Serikali siku ya Jumanne kuwa ya mapumziko ya kitaifa.
Akizungumza wakati wa kutoa ratiba rasmi ya mazishi hayo katika Jumba la Harambe jijini Nairobi, Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua amesema siku hiyo imetengwa ili kuwarusu Wakenya kumwomboleza Hayati Mzee Moi, wakati wa Ibada ya Kitaifa ya wafu.
Aidha, Kinyua amesema mwili wa Hayati Mzee Moi utawekwa katika Majengo ya Bunge, kuanzia siku ya Jumamosi saa nne hadi Jumatatu ili kuwapa fursa Wakenya kuutazama kati ya saa mbili na saa kumi na moja. Kinyua ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati andalizi, amesema Rais Uhuru Kenyatta akiwa Amiri Jeshi Mkuu, ataongoza gwaride maalumu la vikosi vyote vya majeshi, nje ya Majengo ya Bunge kwa heshima ya Mzee Moi siku ya Jumamosi asubuhi.